Posti Maarufu

Thursday, November 11, 2010

MFUMO WA MITIHANI YA VYUO VIKUU HAUTOI NAFASI YA KUWATAMBUA WENYE VIPAJI KWA HAKI

        Nilikuwa  naongea na rafiki yangu mmoja tuliyewahi kusoma naye katika shule moja ya sekondari,kwa sasa  anasoma katika chuo kuu kimoja cha afya ya binadamu  hapa nchini.Mbali na kuongelea matatizo mengi yanayojitokeza katika fani mbalimbali za vyuo vikuu, suala lililonivuta zaidi ni mfumo wa kuwatahini wanvyuo hasa katika mitihani ya mazoezi kwa vitendo.Pale mwanachuo anapofika hatua ya kufanya mitihani ya kliniki kwa upande wa wanavyuo wa vyuo vya afya ya binadamu, anatakiwa  kuchukua maelezo ya mgonjwa ili baadaye awakilishe maelezo hayo kwa yule aliyepangiwa kumsimamia ,hapo ataulizwa maswali ambayo iwapo atayajibu vema atapewa maksi kadha.Njia hii inaweza kuwa ndiyo njia bora kabisa ya kumtahini mwanachuo hasa ukizingatia kuwa inamjengea kujiamini zaidi  katika kusema na kufanya mambo.
       Tatizo kubwa linaloibuka ni tofauti kati ya watahini au “supervisor” wa zoezi hili,labda ni kwa sababu ya wingi wa wanavyuo inakuwa vigumu kwa mtahini mmoja kuwasimamia wanavyuo  wote.Hapo kitengo husika hulazimika kuweka wasimamizi zaidi ya mmoja wenye viwango tofauti vya kielimu na wanaotofatutiana katika kutoa maksi.Kwa mfano iwapo utakutana na Profesa katika mtihani andika umeumia, maana atakuulizauliza vitu vingi sana tofauti na utakapokutana na mtu mwenye degree mbili tu ama ‘specialist’ .Kutokana  na hizi tofauti kati ya watahini na kwa kuwa utoaji wa maksi ni utashi wa msimamizi binafsi hapa linazuka suala ambalo matokeo yake si mazuri kwani iwapo mwanafunzi asiye bora atakutana na specialist akampa maksi nyingi kwa utashi wake binafsi ina maana huyo atakuwa amefaulu sana na kuonekana bora.Labda utasema kama mtu ni bora atakuwa bora tu hata akikutana na Profesa lakini hoja hapa ni kwamba mpaka mtu kuitwa Profesa anakuwa anafahamu mambo mengi sana ambayo atataka umueleze kiprofesa profesa.
         Changamoto nyinyine zinajitokeza katika katika vyuo vingi ni katika kazi za ziada yaani ‘assignments’ ambazo iwapo utampata mwalimu muelewa wa hali halisi ya usomaji utapewa alama za kuchekelea.Changamoto nyinyine ni katika usahihishaji wa mitihani ya kuandika inayohitaji maelezo “essay’ ,siyo siri waulize wanavyuo wengi watakuambia iwapo mwalimu fulani atasahisha mtihani wako utakuwa na nafasi kubwa ya kufaulu na waalimu ambao wakisahisha mtihani wako utakuwa na nafasi ya kutokufaulu wanajulikana pia.
       Tatizo linalojitokeza ni kwamba kwa kuwa wanavyuo katika vyuo kadhaa  hugawanywa katika makundi na wanapangiwa walimu tofauti tofauti wa kuwafundisha ,pale mwanachuo anapokutana na mwalimu ambaye  siyo yule aliyemfundisha kama msimamizi wake katika mtihani au assignments au mitihani ya maelezo marefu (essay) ,kumekuwa na matatizo ya mgongano wa kitaaluma kwani japo elimu na mwongozo wa kielimu ni wa aina moja  lakini kila mwalimu anapenda kumuandaa mwanafunzi kwa utashi wake ambao si lazima mwalimu mwenzake akubaliane nao.
       Labda kwa kuwa watahiniwa ni wengi kuna haja ya kuweka viwango vya kumtahini mwanafunzi,viwango na maelekezo ambayo vitengo husika vitawajibika kuhakikisha kuwa vinazingatiwa katika kutahini wanavyuo la sivyo atumike mtahini mmoja tu pasipo kujali atatumia muda gani kuwasimamia au kusahihisha mitihani ya wanachuo wote wa kozi husika.
     Hii yote ni katika kujaribu kumpa kila mtu kile anachostahili kupata hasa katika utoaji wa tuzo mbalimbali vyuoni.Sisemi kila anayepewa tuzo si bora bali tumekuwa tukishuhudia minong’ono ya chini chini kati ya wanavyuo wakihoji kwa vipi mtu Fulani apewe tuzo.Actually wanavyuo wenyewe wanafahamiana ,wanajua ni nani aliyebora na ni nani asiyebora na iwapo yule ambaye wanavyuo wenyewe katika kozi na mwaka husika wanamkubali kwamba yuko ‘fit’ kimasomo akakosa kutambuliwa kwa tuzo na kupewa mwingine ambaye pengine anaonekana kabisa hayuko ‘fit’ kwa binadamu yeyote mwenye akili timilifu ni lazima atakuwa na walakini.
     Nawapongeza sana waalimu wa vyuo kwa kazi nzuri wanayoifanya.Kwani wamekuwa wakijitahidi kukabiliana na  changamoto za kuongezeka kwa wanavyuo kwa kasi kiasi kwamba wao wanabeba mzigo ambao ni matokeo ya propaganda za kisiasa za kuongeza idadi ya wanaojiunga katika vyuo pasipo kuongeza miundombinu na waalimu.Kwa kuwa suala la kuongezeka kwa idadi ya wanavyuo ni la kisiasa zaidi si ajabu kuwakuta wanavyuo wakisoma wakiwa wamesimama kwa kukosa mahali pa kukaa kutokana na wingi wao na nadhani kwa miaka ijayo wengine watakuwa wanachungulia madirishani kwa pale ambapo hali hiyo haijajitokeza.
      Lengo la makala hii ni kujaribu kueleza hali  halisi ilivyo na kutoa changamoto kwa wakuu wa vitengo vya kielimu kutafuta mbinu iliyobora kabisa ya kuwatahini wanavyuo na kuwatambua waliobora kwa haki.
      Ushauri wa bure kwa wanavyuo ni kwamba lazima kukaza buti kukabiliana na changamoto zozote zinazojitokeza katika  mfumo mzima wa elimu na mitihani.Ni vema ukajiandaa kisawasawa ili ujijengee hali ya kujiamini pasipo kujali utakutana na nani katika mtihani.Kwa kufanya hivyo utakuwa umejiweka katika nafasi nzuri ya kufaulu kwa kiwango kizuri pasipo kujali utapata tuzo au la.
Nawapongeza sana wanavyuo ambao wanasoma kwa bidii sana na hatimaye kupata tuzo mbalimbali kwa kutambua vipaji na bidii zao binafsi katika elimu kwa ujumla .
                             Kaza buti na utavuna ulichopanda
                             
Mwanamtandao

No comments:

Post a Comment