Posti Maarufu

Thursday, November 11, 2010

ABC’ KISU KINACHOPOTEZA MAKALI KATIKA KUZUIA MAPAMBANO DHIDI YA UKIMWI

            Wakati nchi ya Uganda ilipofanikiwa kupunguza maambukizi ya Virusi vya Ukimwi (VVU) katika miaka ya tisini,wataalamu na watafiti waliobobea katika masuala ya magonjwa yanayoambukizwa kwa njia ya zinaa ikiwemo Ukimwi walifurika kwa wingi nchini humo ili kujua mbinu zilizotumika kupunguza maambukizi mapya kushuka kwa kasi ya ajabu.Mojawapo ya matokeo ya tafiti ambazo zilifanyika ilikuwa ni matumizi ya sahihi ya njia ya ‘ABC’ katika kupambana na maambukizi ya Ukimwi.Matokeo ambayo yalipelekea nchi nyingi kuanza kutumia mfumo huo kaatika mapambano hayo.
            ‘ABC’ ni kifupi cha maneno matatu ya kiingereza yaani ‘Abstinence,  Being faithful na Condom using) kwa Kiswahili yakimaanisha Kujiepusha kufanya ngono,Kuwa mwaminifu kwa mpenzi wako na Kutumia Kondomu.ABC imekuwa ikitumika kama njia ya mapambano dhidi ya Ukimwi kwa miaka mingi sasa.Mbinu hii mbali na kuonyesha mafanikio katika nchi kama Uganda , Thailand (iliyoitwa baba wa kondomu kutokana na matumizi ya kondomu kwa kasi)  na nchi nyingine nyingi bado kuna changamoto nyingi zilizojitokeza.
              Changamoto nyingi sana zimejitokeza baada ya maambukizi ya VVU kuendelea kuongezeka kwa kasi katika nchi nyingi ikiwemo Uganda ambayo awali ABC ilionyesha mafanikio.Changamoto kubwa zilizo jitokeza ni pale unapomshauri mtu aache kufanya ngono pasipo kumfundisha mbinu mbadala hasa anapojisikia kufanya ngono.Mimi naamini kuwa hakuna mtu anayeamua kufanya ngono tu kama vile mtu ulivyozoea kuvaa nguo.Ili mtu afikie uamuzi wa kufanya ngono ni lazima kuwepo na msisimko fulani mwilini, kwa maana hiyo pale mtu anapopata msisimko huo ambao pengine anaweza kushindwa kuukabili hadi aamue kufanya ngono na unapomwambia aache au asubiri pasipo kumshauri nini cha kufanya anapopata haja hii,utakuwa hujamshawishi.Hapa sisemi mtu hawezi kuacha kufanya ngono bali naongelea ukweli na hali halisi ilivyo.Changamoto nyingine katika suala hilihili ni pale unapomshauri binti wa Uswahilini kwa mfano,binti ambaye hajaenda shule ama hana ajira maalumu na wazazi wake maisha yao ndiyo hayo.Binti huyu anahitaji kupendeza kwa mavazi,anahitaji chakula,anahitaji vipodozi na kwenda saluni na pengine anahitaji kuwa na simu na matumizi mengine kedekede ya mabinti hasa wa kizazi hiki cha ‘dot com’ na ambapo ‘option’ pekee ya kuvipata vyote hivyo ni kwa kufanya ngono ili apate fedha ya kujipatia mahitaji yake yote ,je unadhani binti huyu ukimwambia aache kufanya ngono asubiri pasipo kumpa mbinu mbadala za kujipatia mahitaji yake ,unafikiri ataacha kweli?.Hapa tunajifunza kwamba mapambano ya Ukimwi si kumwambia mtu aache kufanya ngono tu bali kumpa mbinu mbadala  za kufurahi na mpenzi wake pasipo kufanya ngono,kumfundisha mtu jinsi ya kuzitawala hisia zake na kuzishilikisha sekta zote kikamilifu ili kumwezesha kila mmoja kuwa na njia dhabiti ya kujipatia mahitaji yake na kuondoa umasikini.
  Changamoto pia zimejitokeza katika suala la watu kuwa waaminifu kwa mpenzi mmoja.Fikiria migogoro inayojitokeza kati ya wapenzi na wanandoa.Kwa mfano iwapo mwana ndoa mmoja atagundua mapungufu fulani kwa mwenzake mfano njia  ya kufanya mapenzi na wakishindwa kuwa tayari kuongea kwa uwazi ili kutatua mapungufu hayo  labda kutokana na aibu,mila au hofu ya kufikiria kuwa mwenzio atakuona muhuni ni wazi kwamba utashawishika kwenda nje ya uhusiano kutafuta raha ambayo mwenzio hawezi kukupa,raha ambayo iwapo mngekuwa wawazi na kuongelea matatizo yanayojitokeza hasa wakati wa kufanya tendo la ndoa,mngeweza kutatua na kuboresha mapenzi yenu na kupelekea kuwa waaminifu zaidi. Kutoongelea matatizo katika mahusiano,migogoro kati ya wapenzi na wanandoa  na tamaa za mtu binafsi ambayo pengine ni  kutokana na makuzi  na mfumo wa maisha wa mtu aliyopitia vyote hivi vimeifanya mbinu ya kuwa mwaminifu kwa mpenzi mmoja kushindwa kutekelezeka.Labda sasa kuna haja ya kuwa na wataalamu maalumu wa kushauri wapenzi wanapokuwa na migogoro katika mahusiano (Sexuality counselors) tofauti na hali ilivyo kwa sasa ambapo jukumu hilo limebaki kwa Madaktari (hasa migogoro inapohusisha mabadiliko katika afya ya mtu),Maafisa Ustawi wa jamii( ambao wanahusika zaidi mahusiano yanapovunjika ),Viongozi wa dini,Wanasaikolojia (ambao wameshirikishwa zaidi katika magonjwa ya akili) na Mahakama (pale talaka zinapohitajika).Ukweli ni kwamba kwa kuwa na washauri maalumu ya masuala ya mahusiano wakiwa na ofisi zao tulivu na kwa usiri wapenzi wataongozwa katika kujadiliana mbinu za kutatua migogoro katika mahusiano na hiyo inaweza kuboresha uaminifu kati yao.
       Changamoto kubwa zaidi zimeonekana katika matumuzi ya kondomu,mbali na kupingwa na baadhi ya madhehebu ya dini,kushindwa kujua ni umri gani sahihi wa kuanza kumfundisha kijana kuhusu matumizi ya kondomu,mtazamo hasi katika jamii pale mtu anapoonekana kabeba kondomu katika pochi au mfuko wake.Na mbaya zaidi pale mtu anaposhindwa kutumia anapofikia wakati wa  kuamua kufanya ngono.Imeonekana kwamba suala la mtu kuamua kutumia kondomu hata kama anayo katika mfuko wa suruali au pochi yake aliyoiweka pembeni mwa kitanda wakati anapotaka kufanya ngono ni gumu.Suala la kuamua kuchukua na kutumia kondomu kwa kuunyoosha tu mkono kuifikia kondomu hasa anapokuwa ‘amechemka’,pochi au suruali inaonekana kama vile ipo Marekani yeye yupo Bongo!.Ni wapenzi wangapi wanaoendelea kutumia kondomu hasa baada ya kuaminiana?.Kuna mifano mingi sana inayoonyesha kuwa njia ya ABC ina mapungufu ama walioiharalisha hawakufikiria matatizo ambayo yangeweza kujitokeza hasa katika nchi za uchumi wa aina yetu na kupelekea njia hii kutoleta mafanikio yaliyotegemewa katika kupunguza maambukizi ya VVU kwa maana hiyo ‘ABC’ kama ni kisu kimepoteza makali yake.
        Sisemi ABC isiwepo,acha iendelee kuwepo lakini sasa kuna haja ya kutafuta mbinu mpya kabisa mbali na kile kinachoitwa stadi za maisha.Suala kubwa hapa ni kumwezesha mtu kuchukua uamuzi sahihi pale anapofikiria au anapokuwa katika mazingira ya kufanya ngono.Kumwezesha mtu kutambua kwa undani faida za uamuzi wowote atakaochukua pale anapofikiria kufanya ngono.Awezeshwe kutambua thamani yake,dhumuni la mungu wake kumleta duniani,jukumu lake,malengo na matarajio yake,thamani ya mwili wake na umuhimu wa afya yake kuwa imara ili aweze kuyakabili majukumu yake kama mama au baba pale atakapoamua kuanza maisha ya ndoa.
       Mwanasaikolojia mmoja nchini Thailand aliwahi kusema, ‘Mtu anaposhindwa kutambua faida na hasara za uamuzi wake na mtu huyo kuchukua uamuzi ambao unahatarisha hatima ya maisha na afya yake,basi tayari ni mgonjwa wa akili na anahitaji kuwaona wanasaikolojia ambao hata hivyo hawatamsaidia sana kwani madhara ya uamuzi wake hayawezi kubadilishwa’.
       Tunachojifunza hapa ni kufikiri kabla ya kutenda.
Mwanamtandao

No comments:

Post a Comment