Posti Maarufu

Sunday, November 28, 2010

'NDOA' ZA VYUONI NA MADHARA YAKE KWA WAHUSIKA

“………..nikiwa nimejipumzisha chumbani kwangu,chumba ambacho kipo mahali ambapo kwa lugha ya wenyewe tuyaita ‘Hostel’,ghafla mlango ulifunguliwa kwa kasi ya ajabu,akaingia rafiki yangu ,kabla sijauliza kulikoni  alianza kufoka na machozi yakimtoka.”Najuta sana kumpenda ‘R’,Mapenzi yetu yalikuwa yanaenda vizuri,lakini mara tu baada ya kumaliza ‘University exams’ leo hii nimemkuta na yule jamaa yake wa zamani,yule……………”
      Ni kawaida kwa kijana aliyefikisha umri wa kuamua kile anachoweza kufanya na nani na kwa wakati gani kupewa uhuru huo pasipo kuingiliwa kimaamuzi na mtu yeyote ilimradi tu sheria ya nchi inalindwa.Uhuru huu pia ni pamoja na uhuru wa kuchagua na kumpenda yeyote wa kupendeka kwa sababu zake mwenyewe,si unajua hiki ni kizazi cha ‘DOT COM’ yaani kizazi cha utandawazi,kizazi ambacho mzazi wangu aliyepo kijijini hawezi kunichagulia huko binti wa kuoa nikakubali,huu ndiyo ukweli halisi na lazima tukubaliane nao.
     Kwa wanachuo, kama walivyo vijana wengine,na hata jamii na serikali wanalitambua hilo,wanao uhuru wa kufanya maamuzi yao wenyewe,si mnajua mtu wa ‘Diploma’ au ‘Degree’ ni mtu mkubwa kifikra na hata kiumri?.Hali hii imewapelekea wasomi hawa kuchukua maamuzi ambayo siwezi kuhukumu moja kwa moja kuwa ni mazuri au mabaya kwani nitakuwa nimeingilia uhuru wa vijana kufanya mambo ambayo pengine sisi hatuwezi kujua manufaa yake kwa tathmini ya haraka haraka.
     Uhuru huu wa kimaamuzi umewafanya wanavyuo wanaoishi katika ‘Campus’ ama ‘Hostel’ waamue kuazisha mahusiano kati yao au na watu wengine wa nje ya pale wanapoishi.Ikumbukwe tu kuwa kuna mambo mengi sana yanayomzunguka mwanachuo hasa kayika maisha yake ya kimapenzi.Zipo sababu za kijana wa kiume mwanachuo kuwa na uhisiano na binti wa ‘mtaani’ ambaye si mwanachuo na zipo sababu pia kwa kijana wa kike mwanachuo kuwa na uhusiano na Mwanamume wa ‘mtaani’ asiye mwanachuo.Labda mambo hayo tutayaangalia kwa undani katika matoleo yajayo ya gazeti hili la Familia.Kwa leo tuangalie  mahusiano ya kimapenzi kati ya wanachuo.Si unajua upendo hauchagui ili mradi tu umempenda wa kupendeka?.Mahusiano haya kati ya wanachuo,mengi kati ya aya yamezaa ‘Ndoa’ za haki hasa pale wanazuoni hawa wanapohitimu Degree na Diploma  zao na kuingia mitaani lakini pia si mahusiano yote yanayodumu kwa muda mrefu na baadhi ya watafiti mbalimabali wamebainisha kuwa mahusiano haya yamechangia ‘kuporomoka’ kielimu kwa baadhi ya wahusika na hata wengine hushindwa kuendelea kabisa na masomo yao,sisi tunaita ‘Discontinuation’.Japokuwa inaweza kuwa ni asilimia ndogo tu ya wanaoshindwa  kuendelea na masomo yao lakini lazima tutambue kuwa tayari serikali imewekeza kwa watu hawa kwa mamilioni ya fedha za mikopo wanayopewa.
    Mtafiti mmoja aliyefanya uchunguzi katika vyuo kadhaa hapa nchini,alibainisha kwamba kati ya asilimia arobaini na tisini  na saba ya wanachuo wako katika mahusiano ya kimapenzi ,na kati ya hao,asilimia hamsini hadi sabini wana mahusiano ya kimapenzi kati yao kwa wao na ni asilimia 0.5 hadi 2 tu ndio wanaodumu katika mahusioano hadi mwisho wa masomo yao chuoni na hatimaye kuoana kabisa.Si vibaya kabisa kuwa katika mahusiano ,suala kubwa hapa ni kuwa nini faida au hasara ya mahusiano haya hasa katika nyakati hizi za Ukimwi?
 Mtafiti mwingine alibainisha kuwa kila mwaka takribani asilimia moja hadi tano ya mabinti wanachuo wanapata mimba.Baadhi yao hujifungua na kuendelea na masomo yao na wengine hatujui mimba hizo zinapoishia kwani hatimaye wahusika huendelea na masomo.Bahati nzuri ni kwamba hakuna sheria inayomzuia binti mwenye mimba chuoni kuendelea na masomo si unajua wengine ni wake za watu.
     Faida kubwa zilizoelezwa za kujiingiza katika mahusiano haya zimetajwa kuwa ni pamoja na kupata misaada ya kielimu hasa mitihani inapokaribia na misaada ya  kifedha hasa pale zile za mkopo ‘Boom’ zinzpoisha,kupata  mwenza wa kukuliwaza na kukupa moyo hasa masomo yanapokuwa magumu na kupunguza ‘Academic stress’,kuepuka upweke(msononeko) na kusaidiana kumudu gharama za maisha ya chuo na wengine husema wanajiepusha na ukimwi kwa kuwa na mpenzi mmoja mwaminifu na Wengine husema hii ndiyo njia ya kumpata mke au mme ambaye mnafahamiana na kuzoeana kwa muda mrefu hasa ukiwa katika uhusiano imara.
    Madhara makubwa ya mahusiano haya yamegawanyika kati ya wavulana na wasichana,japo kuna madhara ya jumla kama vile uwezekanifu wa kupata magonjwa ya zinaa,Chuki ‘hate’ kati ya wanachuo hasa pale wanapochangia bwana au binti na kuna ushahidi wa migogoro na mizozano kadha kati ya wanachuo ambayo mingi imehusishwa na kuchangia mpenzi kama chanzo.
    Kwa wasichana mimba za mapema haziepukiki na japokuwa wengine wanavumilia na kuzilea mimba hizo hadi wakajifungua wakati huohuo wakiendelea na masomo yao kama kawaida,kwa wengine uwezekanifu wa mimba hizo kutolewa kwa wakati wowote hauepukiki hasa pale mhusika anapokwepa jukumu lake na hofu ya wazazi au wanachuo wengine kugundua.Mahusiano haya pia yamehusishwa na kuporomoka kielimu kwa mhusika hasa kutokana Stress na migogoro ya kimapenzi inapojitokeza wakati wa mitihani au mitihani inapokaribia,Kupoteza muda mwingi kulea mtoto hasa kwa wale wanaojifungua hayab yote yamepelekea kushuka kwa kiwango cha kufaulu kwa baadhi ya wasomi.
    Kwa wavulana tatizo kubwa linalijitokeza ni kuishiwab fedha mapema kabla ya muda uliopangwa na Bodi ya mkopo kwani japo mnapata mkopo uliosawa mabinti wengi hubana fedha yao hasa wakati kupata chakula na kumuachia mvulana jukumu hilo ili waweze kupata fedha ya ziada kwa ajili ya saluni  na mambo ya urembo si unajua dada zetu wa vyuo wanavyopenda kupendeza?.Madhara mengine kwa wavulana ni kuporomoka kielimu hasa mahusiano yanapovunjika.Kwa kawaida msichana anayekupenda ili apate msaada wa kielimu,uhusiano wenu huimarika pale mnapokaribia mitihani na hulegalega au hata kuvunjika kabisa mara tu mitihani inapoisha.
   Matatizo yanayopelekea kuvunjika kwa mahusiano ambayo mmoja kati ya wapenzi alimpenda mwingine kwa dhati husababisha madhara ya kiakili na hivyo magonjwa kama ‘Depression’ au Post Traumatic Stress Disoder’ Hayaepukiki ambayo huweza kuwa na matokeo mabaya sana kwa mhusika.
 Kwa mfumo huu wa maisha,maisha ya kila mtu kuamua nani wa kumpenda kwa wakati gani na wapi changamoto kubwa zinazoibuka ni kuwa nani awajibike? Wazazi ambao wako huko vijijini ambako ndiko wasomi wengi wanapotokea? Au Waadhiri ambao wajibu wao ni kutoa elimu ya ‘Degree’ au ‘Diploma’ darasani tu na sio elimu ya mahusiano?Je washauri wa wanachuo wanatimiza wajibu wao?Au ni jukumu la wanachuo hawa kutatua matatizo ambayo ni matokeo ya maamuzi yao wenyewe?.Tunaweza kujiuliza maswali mengi ambayo tunaweza tusipate majibu yake kwa haraka,labda tuwaachie hawa wasomi wenyewe kwa kuwa ni watu wazima kifikra na kimwili kuamua kusuka au kunyoa.Kwani kila mmoja anao uhuru wa kupenda au kutopenda na wanavyuo wanajua jema na baya.!!!!!!!!!
  Tukutane wiki ijayo ambayo nitakuletea makala ya kusisimua zaidi.


Imeandikwa na Mwanachama wetu

1 comment:

  1. kiukweli sioni uelimishaji kama hamtoi solution. kusema mwaibua tu sio ishu na kama mko serious mbona kuna issue nyingi za maadili za kuongelea than hizi taarifa nazotoa zisizo na habari ndani yake? hamna jipya nyinyi kajipangeni tu.

    ReplyDelete